Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ameweka wazi utetezi wa Tanzania katika
mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa na Malawi.
Akizungumza na wahariri wa habari katika
semina ya ardhi Dar es Salaam jana, Profesa Tibaijuka alisema tayari
Rais Jakaya Kikwete ametoa ushahidi wa mpaka huo katika Kamati ya Marais
Wastaafu, Festus Mogae wa Botswana, Joachim Chisano wa Msumbiji na
Thabo Mbeki wa Afrika Kusini.
Katika ushahidi huo, kwa mujibu wa Profesa
Tibaijuka, Tanzania ilitumia zaidi historia ya ugawaji mipaka ilivyokuwa
na kutumia ushahidi wa nyaraka za serikali za kikoloni, zilizoshiriki
kugawa mipaka ya Afrika.
Profesa Tibaijuka alisema mipaka ya nchi
iliwekwa mwaka 1890 katika Mkataba wa Wajerumani waliokuwa wakitawala
Tanganyika kwa kutumia hadithi za wagunduzi waliotangulia Afrika, kabla
ya Wakoloni kuanza kugawana bara hilo.
Wakati huo kwa mujibu wa Profesa Tibaijuka,
mpaka kati ya Tanganyika na Kongo na hata Malawi, ulikuwa Mashariki ya
Ziwa na hivyo hata Ziwa Tanganyika, lilipaswa kuwa Kongo.
Alifafanua kuwa katika upimaji, baada ya
kufanya uamuzi huo wa watawala, hatua ya pili ilikuwa kuunda tume kwenda
kuhakiki mpaka huo kwa kuzungumza na wenyeji, na kuurekebisha kwa
kufuata taarifa za wenyeji.
Mwaka 1898 tume hizo zikaundwa, na matokeo yake mipaka Ziwa Tanganyika, Mto Songwe na hata Ziwa Victoria ikawekwa katikati.
Kwa bahati mbaya, mwaka 1914 Vita ya Kwanza
ya Dunia iliibuka na kusababisha tume hizo kusimama kazi kabla ya
kupita na kuthibitisha mpaka katika Ziwa Nyasa.
Profesa Tibaijuka aliendelea kuanika
ushahidi huo, kwamba baada ya vita ya dunia, Ujerumani ilishindwa na
kupoteza makoloni yake ambayo yalichukuliwa na League of Nations ikiwamo
Tanganyika ambayo ilitolewa kwa Uingereza kama mwangalizi.
Tanzania imethibitisha katika ushahidi wake
kuwa, kitendo cha Uingereza kupewa Tanganyika kuwa mwangalizi huku
Malawi ikiwa koloni lake, kilisababisha tume hiyo kutoendelea na kazi,
kwa kuwa hakukuwa na umuhimu wa mpaka, wakati mtawala wa Malawi na
Tanganyika akiwa mmoja.
Kwa mujibu wa Profesa Tibaijuka, Uingereza
ilikuwa ikipeleka taarifa za uangalizi mara kwa mara League of Nations
na kabla ya uhuru miaka ya 1950, Gavana wa Tanganyika alipeleka taarifa
kutaka tume ifanye kazi yake kuhusu mpaka.
Profesa Tibaijuka alisema taarifa hizo ziko
Geneva, Umoja wa Mataifa, na ujumbe wa Tanzania ulilazimika kwenda
kupekua katika maktaba ya Umoja huo kupata vielelezo vya taarifa za
Uingereza kuhusu mpaka, ambazo zimetumika katika ushahidi.
Ushahidi mwingine ambao Profesa Tibaijuka
alisema utaisaidia Tanzania ni makubaliano ya kimataifa yaliyo chini ya
Umoja wa Mataifa kuhusu kugawana eneo la maji.
Alisema kwa kufuata makubaliano hayo, haiwezekani watu wa Mbamba Bay, waombe kunywa maji ya Ziwa Nyasa kutoka Malawi
No comments:
Post a Comment