Mkazi wa Kijiji cha Kihinga, Kata ya Bugarama wilayani Ngara mkoani
Kagera(jina tunalo), anashikiliwa katika kituo kidogo cha polisi cha
kata hiyo baada ya kutuhumiwa kuuza kilo moja ya nyama ya binadamu kwa
Sh100,000.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kihinga, Hassan Mohamed alisema
kuwa jana saa mbili usiku, wananchi walipeleka fedha nyumbani kwake
kununua nyama hiyo na alipowaona alikimbia na wananchi hao kwa hasira
walimkimbiza ili kumuua na hapo hapo kuunguza nyumba yake.
“Mgambo ndio walimnusuru asiuawe na wananchi wenye hasira kali na
alikimbizwa kituo kidogo cha polisi Kata ya Bugarama ili kuokoa maisha
yake “.
Akizungumza na gazeti hili, Kamanda wa mgambo wa kijiji hicho,
Emanuel Kaloli alisema wananchi waliandamana baada ya kusikia taarifa za
kuwapo mtu anayeuza nyama ya binadamu na kutaka kuhakikisha ukweli huo.
Alisema baada ya wananchi kufika, walianza kumshambulia na kutaka
kumuua, lakini wanamgambo wa kitongoji walifika kisha kumuokoa mtuhumiwa
na hatimaye kumfikisha kituo cha polisi kwa ajili ya usalama wake.
“Kijana aliyefahamika kwa jina la Man Balyamwabo mkazi wa Shina la
Kalenge katika kitongoji hicho, ndiye aliyeambiwa kuwa angeuziwa nyama
hiyo ya binadamu na kuleta taarifa katika uongozi wa kijiji ili uweze
kuchukua hatua zaidia”.Alisema Kaloli.
Alisema nyumba aliyounguziwa pamoja na mali iliyokuwamo ndani hasa
maharage, mavazi na vitu vinginevyo inakadiriwa kuwa na thamani ya
Sh2.6milioni. Pamoja na kuwepo kwa tukio hilo, baadhi ya wananchi
walisema mtuhumiwa inasemekana ni raia wa nchi jirani ya Burundi na
alianza kuishi katika kitongoji hicho tangu mwaka 1981 kama kibarua wa
kilimo kwenye mashamba.
Taarifa zinasema kuwa katika kuishi kwake na ndugu yake aliyefahamika
kwa jina la Kahungu walikuwa wakituhumiana kwa uchawi na ilifikia
mahala wakatofautiana na kaka yake ambaye alirejea kwao.
Polisi wilayani Ngara imethibitisha kumpokea mtuhumiwa huyo na kwamba
linafanya mahojiano ya kina kwa kushirikiana na viongozi wa kijiji ili
kubaini ukweli wa tukio hilo
No comments:
Post a Comment