Utata umeibuka kuhusu alipo mfanyabiashara maarufu nchini, Alex Masawe
baada ya kuwepo kwa tetesi kuwa ameachiwa huru huko Dubai, Falme za
Kiarabu (UAE) alikokuwa akishikiliwa.
Masawe ambaye alikamatwa katika uwanja wa ndege huko UAE akitokea Afrika
Kusini, kati ya Juni 20 na 25, mwaka jana, anatuhumiwa kwa makosa
mbalimbali yakiwamo ya mauaji.
Mkuu wa Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) - Tanzania, Kamishna
Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav Babile alikiri kuwapo kwa taarifa
kwamba Masawe ameachiwa huru na hayupo Dubai ingawa bado tawi la
Interpol katika nchi hiyo halijatoa taarifa yoyote.
“Tumejaribu kuwasiliana nao mara kwa mara kuhusu kumrudisha nchini
lakini hawajajibu lolote. Hivi karibuni tuliwasiliana nao lakini
hawajatujibu, kwa hiyo tumebaki na maswali. Kwa kifupi hatujui alipo
hadi sasa,” alisema Kamishna Babile.
Alisema awali, baada ya kukamatwa huko Dubai, Tawi la Interpol Tanzania
lilikuwa linafanya mchakato wa kumrudisha nchini ikiwamo kutuma ombi la
kumrejesha mhalifu nchini, lakini ghafla mawasiliano yakakatika.
“Taarifa zilizopo ni kuwa Masawe ameachiwa huru, kwa vigezo gani hatuelewei,” alisema Babile.
Babile alisema iwapo atakuwa ameachiwa na polisi wa UAE, basi itakuwa
ameachiwa kutokana na sheria za nchi hiyo ingawa bado Tanzania
itaendelea kumsaka kwa udi na uvumba.
No comments:
Post a Comment