TAARIFA KWA UMMA KUHUSU TUHUMA DHIDI YA MWENYEKITI WA TAIFA, FREEMAN MBOWE
FREEMAN MBOWE
Kama mojawapo ya mikakati ya baadhi ya watu wanaotaka kuhamisha mjadala
wa makosa yanayowaandama ya utovu wa maadili na usaliti dhidi ya chama,
hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe amezushiwa
tuhuma zisizokuwa na ukweli wowote zikilenga kumchafua kwa nafasi yake
ya uongozi na kuipaka matope taasisi anayoiongoza;
Tuhuma hizo ni pamoja na;
1.Kwamba Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa mwaka 2005 eti alichukua fedha
kutoka kwa Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono kiasi cha
sh.Milioni 40 ili Mwenyekiti Mbowe asifanye kampeni katika jimbo hilo.
2. Mwaka 2008, eti Mbunge Mkono alimpatia Mwenyekiti wa Chama Taifa,
sh. Milioni 20 kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa Tarime, kisha akazitoa
kwenye chama kama mkopo na akalipwa.
3. Mwaka 2010, wakati wa
uchaguzi mkuu Mbunge Mkono eti alimpatia Mwenyekiti wa Chama Taifa sh.
Milioni 200 kwa ajili ya kampeni za mgombea urais.
4. Mwaka huo
huo wakati wa uchaguzi mkuu, eti Mwenyekiti wa Chama Taifa, alipokea
sh. Milioni 100 kutoka kwa Rostam Aziz kwa ajili ya kampeni.
Idara ya Habari ya CHADEMA, inapenda kusema yafuatayo;
1. Hakuna ukweli hata mmoja katika tuhuma hizo. Ni uongo na uzushi
uliopangiliwa kama moja ya mikakati ya watu wenye malengo ya kutaka
kuilaghai jamii kwamba viongozi wa CHADEMA hawana tofauti na wale wa CCM
na kwamba chama hiki kikuu cha upinzani kinachobeba matumaini ya
Watanzania katika kupigania haki zao na kupinga kila aina ya ufisadi,
kionekane hakina tofauti na chama kilichoko madarakani, ambacho
kimepoteza ushawishi kwa wananchi.
2. Matokeo ya uongo huo ni kutaka kuisaidia CCM na kugeuza mjadala.
3. Idara ya Habari ya CHADEMA inapenda kuuambia umma wa Watanzania
wote, hususan wanachama, wapenzi, mashabiki wa CHADEMA na wapenda
mabadiliko nchini kwamba,Mwenyekiti wa Chama Taifa, ameshawasiliana na
mawakili walifanyie kazi suala hili kwa ajili ya kuchukua hatua za
kisheria.
4. Kwa uhakika tunapenda kuiambia jamii ya Watanzania
wote, hususan wanachama, wapenzi, mashabiki wa CHADEMA na wapenda
mabadiliko wote nchini, kwamba; Chama wala Mwenyekiti wa Chama Taifa,
mahali popote na wakati wowote, hajawahi kupokea msaada wa fedha hizo
kutoka kwa waliotajwa kwa malengo yaliyosemwa.
5. Tungependa
kuwaambia waliozusha tuhuma hizo, ni vyema kama wanapenda kutunza
heshima kidogo waliyobakiza katika jamii kutokana na kuelemewa na mzigo
wa tuhuma za utovu wa maadili na usaliti dhidi ya CHADEMA, badala ya
kugeuka kuwa mabingwa wa kupika uongo, wajibu masuala ya msingi
yanayowaandamana kuhusu mikakati yao ya kuhujumu CHADEMA na viongozi
wake, ambayo iwapo chama kisingeibaini na kuchukua hatua za kinidhamu,
ingesababisha kuua ndoto na matumaini ya Watanzania kufanya mabadiliko
ya kimfumo na kiutawala, kwa kuiondoa CCM madarakani.
6.
Taarifa kuhusu baadhi ya tuhuma katika mkakati huo ambazo zimemlenga
Mwenyekiti wa Chama Taifa, kwa kuhusisha shughuli zake binafsi za
uwekezaji, zitajibiwa kupitia taasisi husika.
Imetolewa leo Dar es Salaam na;
Tumaini Makene
Ofisa Mwandamizi wa Habari- CHADEMA
No comments:
Post a Comment