Sunday, 2 March 2014

TAARIFA KUTOKA IKULU



TAARIFA KUTOKA IKULU (KUHUSU POSHO ZA WAJUMBE WA BUNGE LA KATIBA)!
Katika siku za karibuni, kumekuwepo na habari nyingi, baadhi zenye kuchanganya umma na nyingine hata zikidai kuwa baadhi ya wafanyakazi nchini wanapanga kuandamana endapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete atakubaliana na maombi ya nyongeza ya posho ya Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba .
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu (DPC), inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu habari hizo kama ifuatavyo:
(a) Kwamba Mhe. Rais hajapata kupokea maombi yoyote kutoka kwa Uongozi wa Bunge ya kumwomba aridhie kuongezwa kwa posho ya Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka kiwango cha sasa cha sh. 300,000 (laki tatu)kwa siku hadi kufikia sh. 500,000 (laki tano) ama sh. 700,000 (laki saba) kama ambavyo imekuwa ikivumishwa katika baadhi ya vyombo vya habari.

(b) Na kwamba kwa sababu Mhe. Rais hajapata kupokea maombi ya nyongeza ya posho hiyo, hakuna ongezeko lolote la posho ambalo Mhe. Rais ameliidhinisha.

(c) Kwamba alichopokea Mhe. Rais ni maombi ya Uongozi wa Bunge wa kuomba Mhe. Rais aridhie kufanyika marekebisho katika kiwango cha malipo ya siku kwa Wajumbe hao cha sh. 300,000 (laki tatu) ili posho ya kikao iwe posho ya kujikimu na posho ya kujikimu iwe ndio posho ya kikao.

(d) Kwamba Mhe. Rais amelikubali ombi hilo la Uongozi wa Bunge la kufanyika kwa marekebisho katika mpangilio huo wa posho lakini kiwango cha malipo ya kila siku ya Wajumbe hao kibakie kile kile cha sh. 300,000 (laki tatu) kwa siku. 



(e) Kwamba tayari Mhe. Rais amekwishaujulisha Uongozi wa Bunge kuhusu uamuzi wake huo wa kukubali yafanyike marekebisho lakini kiwango kibakie kile kile cha sh. 300,000 (laki tatu) kwa siku.

(f) Hivyo, Mhe. Rais hajaongeza kiwango cha malipo ya Wajumbe hao kwa sababu hakupata kuombwa wakati wowote kuongeza kiasi hicho.

Ni matarajio ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, kuwa maelezo haya ya ufafanuzi yatasaidia kufunga mjadala ambalo msingi wake kwa kweli umekuwa haupo.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

01 Machi, 2014

No comments: