KANISA la Anglicana Jimbo la Mara
kupitia Kitengo cha Maendeleo ya Jamii wameahidi kusaidia kuchangia
gharama za matibabu za Sumayi Girandi ambaye ni Mwanamke aliyefanyiwa
ukatili wa kukatwa mkono na sehemu za siri na aliyedaiwa kuwa ni mume
wake.
Meneja mradi wa Maendeleo ya Jamii wa
Kanisa hilo docta Theophir Kayombo alitoa ahadi hiyo siku chache baada
ya Mwanamke huyo kutoa ushuhuda wake katika maadhimisho ya siku ya
Wanawake duniani iliyofanyika kimkoa wilayani Bunda.
Alisema Kanisa liliguswa na ukatili
mbaya aliofanyiwa Mwanamke huyo kwa kufuatwa nyumbani kwake usiku akiwa
na watoto wake na kuanza kukatwa sehemu mbalimbali za mwili wake na
kupelekea kupoteza mkono wake mmoja wa kushoto na kuharibiwa jicho.
Kayombo alisema kutokana na rufaa
aliyopewa Mwanamke huyo ya kwenda hospitali ya (KCMC) iliyopo Moshi
Kanisa litatoa msaada wa karibu kuhakikisha anakwenda kufanyiwa matibabu
ya kina ili kurekebisha jicho ambalo limeharibiwa na kumsababishia
maumivu.
Alisema wameguswa na ukatili mbaya
aliofanyiwa na kuona kuna umuhimu mkubwa kama sehemu ya jamii
kuhakikisha wanakuwa karibu na muhanga huyo ili kutoa mchango wao katika
kusaidia tatizo.
"Kwanza tunalaani ukatili huu
aliofanyiwa Sumayi kwa kuvamiwa akiwa nyumbani kwake na huyo aliyekuwa
mume wake na kushambuliwa vibaya kwa mapanga na kupoteza mkono wake wa
kushoto na kuharibiwa jicho moja.
"Licha ya kupoteza mkono tulimsikia
kwenye ushuhuda wake yakwamba aliandikiwa rufaa ya kwenda
(KCMC)tutasaidia suala hilo lakini tunaaiomba jamii ibadilike na
kuachana na matukio ya ukatili ambayo yanapoteza nguvu kazi ya Taifa.
Akitoa ushuhuda wa tukio hilo la
kufanyiwa ukatili katika maazimisho ya siku ya Wanawake duniani mjini
Bunda,Sumayi Girandi alisema usiku wa julai 4 mwaka 2013 akiwa nyumbani
kwake katika Kijiji cha Kunzugu wilayani Bunda alivamiwa na aliyekuwa
mume wake kabla ya kutengana na kumkata kwa mapanga.
Alisema aliyekuwa mume wake
waliyetengana kutokana na tabia akiwa na mwenzake walimvamia ndani ya
nyumba yake na kumkata sehemu mbalimbali za mwili wake na kupoteza mkono
wa kushoto huku jicho moja likiwa limeharibiwa vibaya.
No comments:
Post a Comment