Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,Bernard Membe.
Maamuzi
ya mwisho ya usuluhishi wa mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya
Tanzania na Malawi yanatarajiwa kutolewa kesho na kutwa.
Mchakato wa kesi yake hadi sasa umedumu kwa takribani miaka miwili sasa.
Maamuzi ya mwisho ya usuluhishi huo
yanatarajiwa kufanywa na jopo linaloundwa na Marais wastaafu watatu
kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini na Mashariki mwa
Afrika ambao ni Mwenyekiti waka ni Joachim Chissano (Msumbiji), Thabo
Mbeki (Afrika Kusini) na Festus Mogae (Botswana), huku wakishirikiana na
wanasheria na wataalam wa masuala ya migogoro ndani ya jumuiya hiyo.
Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam
jana, Mkuu wa Kitengo na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Mindi Kasiga, alisema jopo hilo la usuluhishi
wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi, katika Ziwa Nyasa, linatarajia
kutoa taarifa rasmi ya usuluhishi kwa siku mbili mfululizo kuanzia kesho
hadi kesho kutwa katika mji mkuu wa Msumbiji, Maputo.
Mbali na jopo hilo, pia mawaziri wa Mambo
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kutoka nchi za Tanzania na
Malawi, wanatarajia kuhudhuria kikao hicho nyeti cha siku mbili kwa
ajili ya kupokea taarifa hiyo ya maamuzi ya mwisho ya usuluhishi.
Jopo la wataalam na wanasheria wa masuala
ya mipaka toka ndani ya jumuiya hiyo ambao watashirikiana na Marais hao
wastaafu katika kutoa hatima ya usuluhisho huo linaundwa na Jaji Raymond
Ranjeva, Jaji mstaafu wa ICJ; Profesa George Kanyeihamba, Jaji mstaafu
wa Mahakama Kuu ya Uganda na Jaji Baney Afako, Mshauri wa Masuala ya
Sheria kwenye Umoja wa Afrika kuhusu mgogoro wa mpaka wa Sudan.
Wengine ni Profesa Martin Pratt, Mkurugenzi
wa Utafiti wa Jiografia na Mipaka; Dk. Dire David Tladi, Mjumbe wa
Kamisheni ya Sheria ya Umoja wa Mataifa; Miguel Chissano, Kiongozi wa
Chuo kinachoshughulikia mipaka ya Baharini na Nchi Kavu pamoja na Dk.
Gbanga Oduntun, Profesa wa Sheria na Mjumbe wa Kamisheni ya mgogoro wa
mpaka kati ya Nigeria na Cameroon.
Kabla ya kufanyika kwa matukio hayo mawili
mjini humo mwezi uliopita, Tanzania na Malawi kwa nyakati tofauti,
ziliitwa na jopo hilo kuhojiwa juu ya taarifa zao za ushahidi wa umiliki
halali wa ziwa hilo zilizowasilisha kwao na mawaziri wa mambo ya nje na
wa pande hizo mbili Novemba, mwaka jana.
Julai, mwaa juzi, Rais wa Malawi, Joyce
Banda, mara baada ya kuapishwa kushika kiti hicho kufuatia kifo cha
mtangulizi wake, Bingu wa Mutharika, aliibua mgogoro huo kwa kutoa
leseni kwa kampuni mbili za kigeni, kutafuta mafuta katika eneo la Ziwa
ambalo linamilikiwa na Tanzania, kwa madai ya kwamba ziwa hilo lote lipo
upande wake.
Mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na
Malawi, unaotambuliwa na sheria za kimataifa ni ule unaopita kati ya
ziwa hilo, ambao ulianza kutumiwa na raia wa nchi hizo mbili miaka mingi
iliyopita kwa kila upande kumiliki asilimia 50 ya Ziwa.
No comments:
Post a Comment