Watu
saba wameuawa kwa kuchomwa moto ndani ya nyumba katika tukio ambalo
nyumba 18 ziliteketezwa na mbili kubomolewa na wananchi waliodai
wanawaua wachawi katika Kijiji cha Murufiti, Kasulu, mkoani Kigoma.
Polisi wameeleza kuwa tayari watu 17 wamekamatwa kwa kuhusika kwenye tukio hilo.
Miongoni
mwa waliouawa katika tukio hilo lililotokea Jumatatu iliyopita ni John
Mavumba (68) na mkewe Elizabeth Kaje 55 ambao pamoja na wenzao walikuwa
wakituhumiwa kuwa ni washirikina.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi, Josephat John ambaye ni mtoto wa Mavumba,
alisema wazazi wake walichomwa moto na kundi la vijana waliokuwa
wakiwatuhumu kuwa ni wachawi.
Alisema
vijana walikuwa wamebeba mapanga, marungu na kupita katika nyumba
mbalimbali wakifanya mauaji wakisema maneno kwa kurudiarudia kwamba
watawamaliza wachawi kwa kuwaua, ndipo yeye na wenzake walikimbia usiku
huo wakihofia kuuawa.
“Niliporudi
alfajiri niliukuta mwili wa mama ukiwa umbali wa mita 10 kutoka ilipo
nyumba yetu ukiwa umeungua na mwili wa baba ukiwa umeungua ndani ya
nyumba,” alisema John.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Jafari Mohamed alisema mauaji hayo yalitokea
Oktoba 6 kuanzia saa 4:00 usiku katika kijiji hicho.
John
alisema baada ya tukio hilo wanaume wengi wameyakimbia makazi yao
wakihofia kuuawa na kundi la vijana hao. “Kijiji kimebaki na wanawake
tu, wanaume wamezikimbia nyumba zao wanahofia kuuawa,” alisema.
Mohamed alisema mauaji hayo yametokana na imani za kishirikina.
Aliwataja
waliouawa kuwa ni John Muvumba (68), Elizabeth Kaje (55), Dyaba Kitwe
(55), Vincent Ntiyaba (42), Herman Ndabiloye (78), Redempta Mdogo (60)
na Ramadhan Kalaliza (70) wote wakazi wa kijiji hicho.
Alisema nyumba zilizochomwa moto ni 18, mbili zilibomolewa na kufanya jumla ya nyumba 20 zilizoharibika kabisa.
Wakazi
wa kijiji hicho, Zablon Andrew na Eveline Enock walisema kwa nyakati
tofauti kuwa chanzo cha mauaji hayo ni mganga wa jadi aliyefika kijijini
hapo na kupiga ramli akiwataja watu waliouawa kuwa ni wachawi.
Andrew alisema baada ya mganga huyo kuwataja, vijana walikusanyana na kuanza kuwateketeza watu bila huruma.
“Kitendo
hiki kimeturudisha nyuma kimaendeleo kwa sababu nyumba zetu zimechomwa
moto na mazao yetu yameharibiwa,” alisema Andrew.
Hali ilivyo kijijini
Mmoja wa watu aliyechomewa nyumba, Evelyne Msilu alisema sasa kijiji hicho kina askari wengi wanaofanya doria.
“Hali
inasikitisha, tumepoteza ndugu zetu waliouawa, wanaume wengi
wamekikimbia kijiji kwa hofu ya kuuawa na vijana wengine wamekimbia
wakiogopa kukamatwa,” alisema.
Kwa nini ipigwe ramli?
Akisimulia,
Enock alisema kuna kijana mmoja katika kijiji hicho ambaye kazi yake ni
kufyatua matofali aliwaomba vijana wanzake kuwa siku inayofuata
wamsaidie kuyapanga katika tanuru.
Alisema jambo la ajabu ni kwamba walipoamka asubuhi walikuta matofali yamekwishapangwa na haikujulikana aliyefanya kazi hiyo.
Alisema kijana huyo na wenzake waliamini kwamba waliofanya kazi hiyo ni wachawi.
Akisimulia
kisa kingine, Enock alisema siku chache zilizopita kuna msiba ulitokea
kijijini hapo na baada ya mazishi, siku iliyofuata walikuta msalaba
umeng’olewa na haujulikani ulipo, jambo ambalo pia lilihusishwa na
ushirikina.
Ofisa
mtendaji wa kijiji hicho, Ogen Gasper aliyeomba Serikali kujenga kituo
cha polisi kijijini hapo, alisema baada ya kupata taarifa za tukio hilo
alifanya jitihada kubwa kuwapata askari, lakini hawakufika kwa
kilichodaiwa ni kukosa usafiri.
Gasper alisema hilo ni tukio la tatu kwa watu kuuawa kwa kutuhumiwa kuwa ni wachawi, la kwanza likiwa limetokea mwaka 1996.
via>>Mwananchi
No comments:
Post a Comment