Na Anitha Jonas –Maelezo.
SHIRIKISHO la Muziki Tanzania
limetoa pongezi za dhati kwa Bunge Maalum la Katiba lililokuwa
likiongozwa na Mwenyekiti wa Bunge hilo Mhe. Samuel Sitta kwa kuingiza
Ibara tatu katika Rasimu ya Katiba inayopendekezwa huko mjini Dodoma.
Pongezi hizo zilitolewa jana na
Rais wa Shirikisho hilo Bw. Addo November alipokuwa akiongea na
Waandishi wa habari hapo jana huku akisema kuwa Rasimu Inayopendekezwa
imezingatia haki za Wasanii kwa kuingiza Ibara tatu zikiwemo Ibara ya
15, ya 38 (II) na Ibara ya 56, 3 (e) ambazo Ibara hizo zinalinda kazi
za muziki na sanaa zote kwa ujumla.
Bw. November alieleza kuwa
Shirikisho limefurahi kuona kuwa Sheria ya inayohusu masuala ya kazi za
sanaa katika nchini imeanza kutekelezwa Kikatiba kama ilivyo katika nchi
mbalimbali zikiwemo Marekani, Rwanda na Uingereza.
“Kwa kubainisha ibara hizi katika Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa, zinaonyesha ulindaji wa Hati Miliki(Intellectual property)
za Wasanii na kazi zao na hii itasaidia kuboresha maisha ya wasanii
kimapato kwa kupitia kazi zao kwani Katiba hii itawalinda wasanii
Kisheria”, alisema November.
Aliongeza kuwa Shirikisho
limeingia Mkataba na Kampuni ya JB Belmont kwa kuweza kuwapatia wasanii
na waandishi wa habari punguzo la bei katika huduma mbalimbali
zinazotolewa na kampuni hiyo.
Aidha, November aliwashauri
waandishi wa habari kuunda Shirikisho la Waandishi wa habari la muziki
kwani hii itasaidia kupata na kutoa taarifa mbalimbali kwa jamii
zinazohusu masuala ya muziki kwa kuaangalia walikotoka na wanakoelekea
kimaendeleo.
Naye Meneja Mahusiano wa Kampuni
ya JB Belmont, Bi. Gillian Macheche alisema kuwa kutakuwa na punguzo la
asilimia 40 kwa huduma mbalimbali ikiwemo kukodi Ukumbi wa Mkutano,
Vyumba vya kulala wageni, vyakula na Vinywaji kwa wasanii na waandishi
wa habari.
Kwa upande mwingine Mjumbe wa
Shirikisho hilo ambaye pia ni Mwanamuziki mkongwe nchini Bw. Kassim
Mapili alitoa shukrani zake za dhati kwa waandishi wa habari kwa kutoa
taarifa kwa umma juu ya afya yake pamoja na jamii kwa ujumla kwa
kumsaidia katika kipindi chote alichokuwa akitibiwa ugonjwa wa Moyo
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
No comments:
Post a Comment