Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Hiiti Sillo
(kushoto) akiwaonyesha waandishi wa habari wakati wa mkutano Dar es
Salaam, bidhaa za chakula na vinywaji walizokamata kwenye maduka makubwa
(supermarkets) ambazo hazifai kwa matumizi ya walaji. Kulia ni
Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula wa TFDA, Raymond Wigenge
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imefunga maduka makubwa
(supermarkets) 29 kwa makosa ya kufanya biashara bila vibali mpaka pale
yatakapotimiza masharti ya sheria.
Pamoja na hatua hiyo, pia TFDA imekamata bidhaa za aina tofauti za maziwa ya watoto ambazo hazikuwa na sifa ya kuuzwa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo, Hiiti Sillo alisema hatua hiyo
imefikiwa baada ya kufanya operesheni kali ndani ya jiji.
“Wakati wa operesheni iliyoanza Machi 10 hadi 21, tulibaini maduka 39 yasiyosajiliwa na mamlaka na tukayaagiza kufunga.
Hata hivyo, kumi kati ya hayo yalitekeleza masharti haraka na kuruhusiwa kuendelea na biashara,” alisema Sillo.
Miongoni mwa maduka yaliyofungiwa ni Puma
Supermarket, ambayo meneja wake, Jackson Kessi alipoulizwa kuhusu uamuzi
huo, alisema anaendelea kutekeleza amri ya TFDA ya kutimiza masharti ya
usajili.
“Mpaka sasa tumeshajaza fomu za usajili na ukaguzi
na kuzilipia. Na tayari tumeshapata hati ya malipo. Tunachosubiri ni
taratibu nyingine zinazofuata za usajili,” alisema, Kessy.
Maziwa ya watoto
Katika hatua nyingine, TFDA imekamata makopo 591
ya maziwa ya watoto yenye thamani ya Sh17.6 milioni ambayo
hayajasajiliwa kwa matumizi hapa nchini.
“Jumla ya maduka 36 yamekutwa yakiuza maziwa ya
watoto ambayo hayajasajiliwa na TFDA. Maziwa hayo ni SMA1, 2 na 3,
Promil Gold, S-26 Gold, Nursoy, Progress Gold, Cow and Gate, Isomil 2,
Infacare Soya, Nutrikids na Aptimil 1,” alibainisha Sillo.
Aliongeza Watanzania wanatakiwa kujua kuwa maziwa
yoyote ya watoto yasiyoandikwa kwa lugha za Kiingereza na Kiswahili
hayastahili kuwapo nchini kutokana lugha nyingine kutoeleweka na
wananchi.
“Bidhaa zote hizo tulizozikamata tutaziharibu na zile
zisizoandikwa kwa lugha za Kiingereza na Kiswahili tutaangalia kama
tutazirudisha kwenye nchi zilikotoka,” aliongeza Sillo.
Pamoja na kutosajiliwa, mamlaka hiyo ilibaini pia kuwapo kwa bidhaa zilizoisha muda katika maduka 23.
Kwa mujibu wa Sheria ya Chakula na Dawa sura namba 219, bidhaa za chakula na dawa zisizosajiliwa haziruhusiwi kuwapo madukani.
Pia sheria hiyo inaitaka TFDA kubaini na kukamata bidhaa zote zilizovunja masharti ya sheria
No comments:
Post a Comment