Thursday, 24 April 2014

MWENYEKITI WA CHADEMA AFUNGWA MIAKA 7 KWA KUJERUHI KILABUNI

Mwenyekiti wa CHADEMA Ezekiel King akiteta jambo na jamaa zake mara baada ya kuhukumiwa kwenda jela miaka 7 kwa kosa la kumjeruhi mtu kilabuni
Askari polisi wakimsindikiza Mwenyekiti wa CHADEMA baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 7 jela

Mmoja wa jamaa waliohudhuria mahakamani akimwaga machozi baada ya Mwenyekiti wa CHADEMA mtaa wa Itiji kuhukumiwa kifungo  cha miaka 7 kwa kujeruhi
 MWENYEKITI wa serikali ya Mtaa wa Itiji Jijini Mbeya mkoani Hapa anayewakilisha (CHADEMA) Ezekiel King(52) na mwenzake Antony Simon(53) wamehukumiwa kwenda jela miaka 7 kutokana na makosa ya shambulio na kumdhuru mwili Nicholaus Mwakasinga(56) mkazi wa Itiji mjini humo.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu mkazi wa mahakama ya Mkoa wa Mbeya Maria Batulaine, mbele ya mwendesha mashtaka wa serikali Juliana William alisema kuwa washitakiwa kwa pamoja walimshambulia Mwakasinga kwa kumpiga na kumjeruhi kichwani na mkononi wakati wakiwa katika kilabu cha pombe za kienyeji kilichopo mtaa wa Itiji.

Alisema anawatia hatiani washitakiwa hao kutoka na kuwepo kwa mashaka juu ya ushahidi wa watu watatu  upande utetezi kugongana na hivyo kuridhika na ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka na hivyo kuwatia hatiani na kwamba hata hivyo wanayo fursa ya kukata rufaa iwapo hawajaridhika na hukumu iliyotolewa.

Akitoa mifano ya kesi  mbalimbali zinazoshabihiana na kesi hiyo Hakimu Batulaine alisema kuwa makosa hayo ni kinyume cha kifungu sheria  cha kanuni ya adhabu namba 225 sura ya 6 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Hakimu Batulaine alisema kuwa katika maelezo ya shahidi namba moja Mwakasinga  ambaye ndiye mlalamikaji  ni kwamba alijeruhiwa na kuumizwa na washitakiwa alipoingia katika kilabu cha pombe za kienyeji na  kwamba alifanyiwa hivyo baada ya kuingia ndani ya kilabu hicho na kusukumwana kuanguka nje.

Alisema katika maelezo hayo shahidi namba moja hadi namba tatu wa upande wa mashtaka walitoa ushahidi unaofanana lakini maelezo ya mashahidi wa upande wa utetezi yanajichanganya na hivyo kutoa mashaka juu ya utetezi wao.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mlalamikaji Mwakasinga alipigwa na kujeruhiwa na washitakiwa na baadaye washitakiwa hao walimchukua na kumpeleka kituo cha Polisi wakidai kuwa mlalamikaji Mwakasinga alikuwa akifanya vurugu kilabuni
.
Hata hivyo mlalamikaji ambaye alilazwa katika hospitali ya rufaa wodi namba nne ambayo hulazwa watu wenye ugonjwa wa akili ili kumpima kama alifanya vurugu kutokana na ugonjwa wa akili alipotoka alifungua mashtaka ya kupigwa na washitakiwa hao ambao walikamatwa na kufunguliwa kesi ya kudhuru mwili.

Katika utetezi wake kabla ya kutolewa hukumu Mshitakiwa King aliomba mahakama impunguzie adhabu kutokana na kuwa na watoto sita na kuwa hakujua kama kitendo cha yeye kama kiongozi wa mtaa kuamka kwenda kwenye tukio kingemtia hatiani

No comments: