
Kauli ya Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January 
Makamba, kwamba, Tanzania inahitaji kiongozi kijana katika nafasi ya 
urais mwenye fikra mpya katika uchaguzi mkuu ujao, imeelezwa kuchochea 
mtafaruku ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa.
Katibu Mwenezi wa Itikadi na Siasa wa (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, 
Charles Shigino, alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari 
jana.Alisema usemi huo ni kuleta siasa za ubaguzi ndani ya chama. 
Shigino alisema CCM inapiga vita ubaguzi wa aina yoyote ndani ya chama 
na kuongeza kuwa kauli ya Makamba ni silaha tosha ya kukivuruga chama, 
hivyo anapaswa kuomba radhi.
“Kauli ya Makamba siyo ya kiungwana. Nadhani aliropoka, hakufikiria 
anachokisema. Na katika nchi hii ndiyo imekuwa ikiongozwa na wazee ndani
 ya miaka mingi na kuwa katika mstari mnyoofu.
Hivyo, wazee wanapaswa kupewa heshima zao na kijana huwezi kufanya jambo la maana bila ya kuwa na mzee nyuma yako,” alisema.
Aliongeza: “Katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia siyo kwamba, 
nchi ndiyo itawaliwe na vijana tena katika nafasi nyeti ya urais. 
Makamba anatakiwa kujitathmini mara mbili mbili. Wazee ndiyo nguzo ya 
nchii hii. Wanaifahamu tokea enzi za uhuru. Sisi tumekuta historia tu.”
“Kama kweli Makamba kama ana nia ya urais, ni bora akajipa muda wa 
kujifunza na kupata uzoefu wa kutosha wa nafasi ya uongozi katika nafasi
 hiyo. Kwani Watanzania wanajua bila ubishi kuwa katika nafasi ya 
uongozi ndani ya CCM hana muda wa mwaka mmoja na nusu.”
Alisema kisiasa Makamba bado ni mdogo na kwamba, anatakiwa kwenda 
kujifunza kutoka kwa wazee waliopo ndani ya CCM, ambao yeye amekuwa 
akiwadharau.
Shigino alisema Makamba anatakiwa kujua kuwa Watanzania wanapomchangua 
mgombea urais kupitia CCM ndiye huyo huyo atakayekuwa Mwenyekiti wa CCM 
Taifa.
Alisema kwa sasa taifa lilipofikia linatakiwa kuongozwa na kiongozi 
mwenye maamuzi ya kutosha pamoja na uzoefu wa kukabiliana na changamoto 
zilizopo, hasa katika nyanja ya uchumi, mendeleo ya jamii pamoja na 
siasa yenye utawala bora.
CHANZO: NIPASHE
 
No comments:
Post a Comment