
KIONGOZI
 wa Taasisi ya Answaar Muslim Youth Centre Kanda ya Kaskazini, Sheikh 
Sudi Ally Sudi, amejeruhiwa kwa bomu la kurushwa kwa mkono akiwa 
nyumbani kwake Mtaa wa Majengo jijini Arusha.
Aidha, mkazi wa Sinza jijini Dar es Salaam, Muhaji Hussein (38), 
alipatwa na mkasa huo akiwa nyumbani kwa Sheikh Sudi akitokea safarini 
Nairobi, Kenya.
Katika mkasa huo, Muhaji alivunjika mguu wa kushoto na kukatika vidole vitatu vya mguu wa kulia kutokana na mlipuko huo.
Ilielezwa kwamba, watu wasiojulikana walivunja kioo cha dirisha usiku 
huo kisha kurusha bomu hilo hadi sehemu walipokuwa wamekaa watu hao.
Hata hivyo, familia ya Sheikh Sudi imesalimika kutokana na kuwa katika 
chumba kingine ambacho hakikuathiriwa haraka na mlipuko huo.
Akizungumza katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru alipolazwa,
 Sheikh Sudi alisema tukio hilo lilitokea wakati wakiwa wanajiandaa kula
 daku akiwa na mgeni wake, Muhaji.
Sheikh Sudi akizungumza kwa taabu kitandani alipolazwa katika wodi ya 
majeruhi alidai kabla ya tukio la bomu tayari alishaanza kupokea vitisho
 vya kupoteza maisha ikiwamo kutishiwa kwa risasi.
“Nimetishiwa mara kadhaa kabla ya tukio hili nilisharipoti katika vyombo
 vya dola, ila wameniumiza sana bila sababu,” alisema Sheikh Sudi.
Majeruhi mwingine Muhaji ambaye ana majeraha makubwa maeneo yake ya 
miguu kuanzia chini ya magoti alisema anamshukuru Mungu kwa kumlinda 
katika tukio hilo.
“Hapa nilipo nimepata majeraha makubwa katika miguu yote miwili, ambapo 
mguu wa kushoto umevunjika na mguu wa kulia kidole gumba na vidole 
viwili vinavyofuata vimekatika,” alisema Muhaji na kuongeza:
“Kabla ya mlipuko mwenyeji wangu alikuwa anasimulia jinsi anavyopokea vitisho wakati huo mtoto wake alikuwa akiandaa chakula.
“Bahati mzuri mtoto alikuwa ameshamaliza na kuondoka tulipokuwa ndipo 
nikasikia kishindo cha kuvunjwa kioo cha dirisha kilichofuatiwa na 
mlipuko,” alisema.
DAKTARI WA ZAMU
Kwa upande wake daktari wa zamu katika wodi ya majeruhi, Leo Temba, 
alisema hali za majeruhi wote wawili inaendelea vizuri na tayari 
walishawapatia huduma zote muhimu.
Akimzungumzia Muhaji alisema ndiye majeruhi aliyekuwa na hali mbaya 
zaidi kutokana na kuvuja damu nyingi, hata hivyo baada ya kupatiwa 
matibabu anaendelea vizuri.
“Wagonjwa wangu mpaka wakati huu wanaendelea vizuri, tumefanya jitihada kuokoa maisha yao. Tumewaongeza damu hasa Muhaji.
“Wote tumesafisha vidonda na kuondoa mabaki yote ya chumachuma na kufunga vidonda ili kuepusha damu kuvuja kwa wingi.”
“Muhaji ndio yuko ‘serious’ amevunjika mguu wa kushoto na una vidonda 
vikubwa ambavyo tumevifunga na tutavishona. Lakini pia mguu wa kulia 
umeumia kwani vidole vitatu vimekatika, gumba na vidole viwili vya 
katikati,” alisema Dk. Temba.
MKUU WA MKOA
Akiwa hospitali kuwatembelea majeruhi Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa 
Mulongo, aliliambia MTANZANIA Jumamosi kuwa uchunguzi wa awali 
umebainisha mlipuko huo hauna uhusiano wowote na vikundi vya kigaidi vya
 Al- Qaeda wala Al- Shabaab.
Magessa alisema kwamba upo mgogoro baina ya waumini wa taasisi za dini 
ya Kiislamu katika Msikiti wa Qiblatein Kandahari eneo la Soko la 
Kilombero jijini Arusha.
“Lipo tatizo la ndani kati ya waumini wa Kiislamu kwani Sheikh Sudi 
ametuambia tayari alishapokea vitisho kutokana na kukataa kutumiwa kwa 
msikiti huo na makundi ya siasa kali yanayoongozwa na Answar Sunna.
“Tunaendelea kuwasaka vijana hawa tutawakamata wote na kuwafikisha mbele ya vyombo ya sheria,” alisema Mulongo.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, 
akizungumzia tukio hilo akiwa Hospitali ya Mount Meru alithibitisha 
kutokea kwa tukio hilo akisema Jeshi la Polisi litahakikisha 
linawakamata watuhumiwa wote.
“Pale msikitini kuna msuguano mkali kati ya waumini wenye msimamo mkali 
na wasio na msimamo mkali. Tupo kazini kuwasaka wote waliohusika na 
kitendo hiki,” alisema Kamanda Sabas.
Kutokea kwa tukio la Sheikh Sudi kurushiwa bomu akiwa nyumbani kwake 
linakuwa tukio la tano linalohusiana na matukio ya ulipuaji wa mabomu 
jijini Arusha.
Tukio la kwanza la mlipuko wa bomu kutokea jijini Arusha lilikuwa ni 
katika Kanisa la Katoliki Parokia ya Mtakatifu Joseph 
Mfanyakazi,Olasite, kisha kufuatiwa na mlipuko wa bomu la nyumbani kwa 
Katibu wa Bakwata Mkoa wa Arusha.
Baada ya hapo mlipuko mwingine wa bomu ulitokea kwatika mkutano wa wa 
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), viwanja vya Soweto kisha 
kufuatiwa na mlipuko wa bomu katika Bar ya Arusha Night Park (a.k.a 
Matako Bar).
Mlipuko mwingine sasa unakamilisha idadi ya milipuko mitano ya mabomu 
kutokea jijini Arusha ni huu wa juzi ambapo Sheikh Sudi na mgeni wake 
wakiwa nyumba usiku walirushiwa bomu lililowajeruhi miguuni.
Kutokea kwa milipuko yote hiyo kulisababisha kupoteza kwa uhai wa watu 
ambao jumla ya watu tisa walipoteza maisha yao kutokana na milipuko hiyo
 huku majeruhu wa milipuko yote wakifikia zaidi ya 120,  ambao kwa 
nyakati tofauti walikuwa wakipatiwa matibabu na kuruhusiwa kuondoka.
 
No comments:
Post a Comment