Rais wa Baraza Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa |
Akisisitiza jambo |
BARAZA
la Maaskofu Katoliki Tanzania limewatoa hofu watanzania katika tamko
lake lingine kwa Bunge Maalumu la Katiba (BMK) likisema haliko nyuma ya
viongozi wala chama chochote cha siasa kama baadhi yao wanavyofiki.
Akitoa
tamko hilo mjini Iringa jana, Rais wa Baraza hilo ambaye pia ni Askofu
Mkuu wa Jimbo Kuu la Iringa, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa alisema;
“Baraza la Maaskofu Katoliki halina chama katika hili, lakini pia halina
mtu au mwanasiasa au chama linachokifanyia kampeni kwa ajili ya
Uchaguzi Mkuu wa mwakani.”
Katika
Jubilei ya miaka 25 ya uaskofu wa Askofu Ngalalekumtwa iliyofanyika
mjini Iringa hivi karibuni, Makamu wa Rais wa Baraza hilo, Askofu
Severine Niwemugizi alitoa tamko kuhusu mchakato huo kwa kuwataka Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kurudi katika bunge hilo bila masharti.
April
16, mwaka huu, wajumbe wanaounda umoja huo, waliamua kutoka nje ya
bunge hilo wakipinga kile wanachosema ni kupuuzwa kwa makusudi maoni ya
wananchi wanaotaka muungano wa muundo wa serikali tatu kama
ilivyopendekezwa katika rasimu hiyo.
Katika
tamko hilo Askofu Ngalalekumtwa alisema; “katika ujumbe wetu wa
kichungaji wa Pasaka 2014, sisi maaskofu Katoliki Tanzania tuliwaandikia
barua watu wote wenye mapenzi mema kwa nchi yetu tukiwaalika kuchukulia
maanani mchakato wa kuandika katiba mpya.”
Alisema
“wakati huu tunawaalika watanzania wote kwa pamoja, tuungane
kuwakumbusha wale waliopewa dhamana ya kukamilisha Rasimu ya Pili ya
Katiba kuwajibika binafsi na katika maridhiano kutupatia katiba
maridhawa.”
Alisema
wajumbe wa bunge hilo wanapasa kujadili kwa umakini kila kilichopo
katika rasimu hiyo ili wafikie muafaka utakaoenzi ujasiri wa kipekee wa
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete wa kuanzisha
mchakato huo.
“Tunawaasa tukiwaombea dhamiri zao zipate maoni mapya ili waweze kubeba kikamilifu dhamana hiyo waliyokabidhiwa,” alisema.
Askofu
Ngalalekumtwa alisema baraza la maaskofu katoliki linawataka wajumbe
wa bunge hilo kuwa wamoja na kufanya kazi yao kwa mtazamo usioegemea
siasa za vyama.
Alisema
ni mategemo yao majadiliano yatafanyika kwa kuheshimiana, kutumia hoja
za kizalendo na kiungwana na kuyaangalia kwa mapana mambo na masuala
makuu yaliyopendekezwa katika rasimu hiyo.
“Kuandika
katiba ni kazi iliyo ngazi ya juu zaidi ya siasa za vyama, na hivyo
utashi wa kisiasa wa kuunda katiba mpya kwa kuzingatia Rasimu ya Pili
utaweza kuridhiwa kwa kuzingatia msingi huu,” alisema.
Alisema
kwa kadri nchi iliyivyo hivisasa kuna sababu za kutosha za kutaka
Katiba mpya zikiwa ni pamoja na ufisadi, wananchi kujisikia kukosa
usalama na amani, nchi kutokuwa na dira na tunu msingi.
“Na
kwahiyo tunawasihi kwa mara nyingine tena ninyi wajumbe wa bunge hilo
kurejea katika sehemu ya pili ya mjadala hapo mwezi Agosti mkiwa na moyo
na mtazamo mpya,” alisema.
Alisema
kwa kazi hiyo wajumbe hao watawasaidia watanzania waendelee kujivunia
kuwa na taifa adilifu lenye amani na linalofanya kazi kwa pamoja kwa
ajili ya manufaa na ustawi wa wote.
Alisema
ikiwa matokeo yatakuwa yenye kuleta mema na kuimarisha amani na utulivu
wa nchi, watanzania wote watawashukuru na kuwasifu na kama tunda la
kazi ya bunge hilo litakuwa ni lenye kuingiza nchi katika matatizo
zaidi, kuwataabisha wananchi na kukosa maelewano baina yao, basi
watanzania watawahukumu na kuwawajibisha kwa kukosa umakini katika
jukumu hilo muhimu mlilokabidhiwa.
Askofu
Ngalalekumtwa alisema nchi haiko tayari kurudi nyuma na kuendelea na
maisha yanayoongozwa na Katiba ya 1977 kwahiyo mahitaji ni kuwa na
katiba itakayowezesha ushiriki kamili wa watu katika maamuzi na
vipaumbele vya maendeleo ya Taifa.
“Tunataka
Katiba ambayo inaruhusu utawala wa sheria, haki sawa kwa wote, manufaa
na ustawi kwa wote na kuheshimu utu wa kila mmoja. Katiba shirikishi
katika matumizi ya madaraka ili yatumike katika kuhudumia wote badala ya
wachache na inayoweza kuzuia matumizi mabaya ya madaraka na ufisadi,”
alisema.
Alipoulizwa
msimamo wake nini kuhusu muundo wa serikali, Askofu Ngalalekumtwa
alisema; “siwezi kusema popote pale, naogopa kuwapa ushawishi watu wetu
na ndio maana msimamo wa kanisa ni kuwataka wajumbe wote warejee,
wajadiliane na kutuletea katiba itakayokuwa na sifa hizo.”
No comments:
Post a Comment