Wakati
akimpa mama yake, Sanura Kassim ‘Sandra’ gari la Sh. milioni 38 huku
akitawanya mamilioni ya fedha kwenye matukio mbalimbali, staa wa Bongo
Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ anadaiwa kunyemelewa na laana
kufuatia baba yake, Abdul Jumaa kuugua na kuvimba miguu bila msaada
wowote.
Staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ akila ujana na mpenzi wake Wema Sepetu.
Kwa mujibu wa chanzo makini cha Ijumaa, baba wa staa huyo anayeishi
Magomeni-Kagera jijini Dar, amekuwa akisumbuliwa na tatizo la kuvimba
miguu na hakuna msaada wowote anaoupata kwani chanzo cha mapato
anachokitegemea ni kodi tu ya nyumba ambayo anaipata kutoka kwa
wapangaji wachache alionao.
BOFYA HAPA KUKISIKIA CHANZO
“Yaani tunashangaa kusikia Diamond ana
fedha nyingi, juzikati tuliona katika gazeti kamnunulia mama yake gari
la milioni 38 (Toyota Lexus-Harrier) sasa kwa nini asimthamini baba yake
hata kidogo?
“Ukweli ni kwamba baba Diamond anasumbuliwa na tatizo la miguu kuvimba.
“Amekuwa akilalamika mara kwa mara lakini Diamond hatujawahi kumuona,”
kilinyetisha chanzo hicho na kuongeza:“Juzikati hapa baba Diamond
alishikika kwelikweli miguu, akaugulia mwenyewe ndani pasipo kuwa na
msaada wowote tena nasikia mzee huyo hataki hata kuongelea lolote kuhusu
Diamond maana haoni umuhimu wa kufanya hivyo wakati amemsusa muda mrefu
sana.”
MATIBABU HAYAZIDI MILIONI
Katika aya nyingine, chanzo hicho kilidai
kwamba ugonjwa wa miguu ambao unamsumbua mzazi huyo, gharama za
matibabu haziwezi kufikia hata shilingi milioni moja za madafu achilia
mbali mamilioni anayoyatapanya staa huyo.
Mama yake Diamond,Sanura Kassim ‘Sandra’ akilitesti gari alilokabiziwa na Mwanaye kama zawadi.
“Ingekuwa tatizo kubwa sana, hapo sawa, kwa sababu miguu huwa inamvimba
lakini akipata dawa za kutumia huwa inarudi katika hali ya kawaida, kwa
nini lakini anamfanyia hivyo baba yake? Amemkosea nini?” Kilihoji chanzo
hicho.
UTAJIRI WAKE WAANIKWA
Wakati chanzo hicho kikiweka nukta hapo
kwa muda, mapaparazi wetu walipewa malalamiko mengine kutoka kwa jirani
mmoja wa baba Diamond ambaye alimsihi amsaidie mzazi wake kwani anaamini
uwezo anao kupitia kumbukumbu ambazo Diamond mwenyewe alizithibitisha
kupitia vipindi mbalimbali vya runingani kama Take One na Spora Show vya
CloudsTV.
Pia kwenye vyombo vingine vya habari zikiwemo redio na magazeti pendwa ya Global Publishers.
Jirani huyo alidai kwamba mwaka jana
Diamond alitangaza kuwa ana utajiri wa Sh. bilioni moja ikiaminika
kwamba mwaka huu umeongezeka mara dufu.
“Nakumbuka mwaka jana kupitia Kipindi cha Spora Show na kile cha Take
One, Diamond alikiri kuwa ana mkwanja usiopungua bilioni moja, hiyo
ilikuwa kwa mwaka jana, sasa mwaka huu unadhani atakuwa na shilingi
ngapi? Aache hizo bwana, amsaidie baba yake hata kwa kumpa mtaji mdogo
wa biashara ambao unaweza kumsaidia,” alisema jirani huyo.
MATANUZI YA DIAMOND, WEMA
Katika kuendelea kuichimba habari hiyo,
mapaparazi wetu walinasa malalamiko kutoka kwa jirani mwingine wa mzazi
huyo ambaye alieleza masikitiko yake kwa kulinganisha starehe ambazo
staa huyo anazifanya na asali wake wa moyo, Beautiful Onyinye, Wema
Isaac Sepetu na maisha halisi ya baba yake.
“Mimi ni mfuatiliaji mzuri wa habari za
mastaa, naona kila siku kwenye vyombo vya habari jinsi gani Wema na
Diamond wanavyotumia fedha nyingi katika masuala ambayo hayana ulazima
kiivyo.
“Sisi kama majirani hatupendezwi na hali
hii, angekuwa anakuja angalau siku mojamoja kumuona baba yake kuliko
kila siku kumhudumia mama yake pekee,” alisema jirani huyo.
Baba yake Diamond, Abdul Jumaa akitafakari jambo.
TATIZO NI NINI?
Mapaparazi wetu waliingia mzigoni kusaka
kiini halisi kwa nini Diamond amwage fedha nyingi kwa mama yake pasipo
kumkumbuka japo kiduchu baba yake ambapo ilielezwa kuwa staa huyo wa
Mdogomdogo hakuwa na ugomvi wowote na mzazi wake huyo.
“Kama ni ugomvi ulikuwepo kati ya mama na baba lakini Diamond hahusiki,
tunashangaa kuona kama staa huyo naye anaweza kumsusia baba yake,”
kilieleza chanzo na kuongeza:
“Mbaya zaidi nasikia Diamond amekuwa mzito kupokea simu za baba yake,
sasa huoni kama siyo jambo la busara, mzazi ni mzazi tu hata iweje. Kwa
mtazamo wangu kinachofuata ni laana.
“Kuna mifano ya watu wengi ambao
waliingia kwenye laana za wazazi wao na wakajikuta kama siyo kufulia
kama (wanatajwa mastaa waliofulia wa muziki Bongo) au hata kukutwa na
umauti.
“Jambo hili si la kibinadamu tu, kwa wale
wanaosoma vitabu vitakatifu watakuwa na mifano mingi ya watu
waliowakosea wazazi wao wakalaaniwa.”
BABA DIAMOND ANASIKITISHA
Ijumaa lilipomtafuta baba Diamond kwa
njia ya simu aliongea maneno ya kusikitisha huku akikataa katakata
kumzungumzia kijana wake huyo.
“Jamani naomba mumuache Diamond na maisha yake, sitaki kabisa kusikia
habari zake maana hata nikiongea naonekana najipendekeza kwake.
“Namshukuru Mungu, kama ni kuumwa kwa sasa naendelea vizuri na maisha yangu, niacheni nipumzike,” alisema mzee huyo kwa unyonge.
DIAMOND ANASEMAJE?
Alipotafutwa Diamond ili kumsikia
anazungumziaje madai hayo, simu yake iliita bila kupokelewa. Tunaamini
atasoma habari hii hivyo si vibaya akatutafuta ili afunguke kwa upande
wake.
MAONI YA MHARIRI
Diamond ni staa mkubwa kwa sasa ndani na
nje ya Bongo, uwezo alionao kifedha unapaswa kuendana na baraka za
wazazi wa pande zote mbili. Vitabu vya Mungu vinatufundisha kwamba
wazazi ndiyo Miungu wetu hapa duniani hivyo hata kama kuna kosa
amefanya, mzazi atabaki kuwa mzazi tu. Hatutakiwi kumkosoa!
No comments:
Post a Comment