SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Freeman Mbowe, kuwekewa pingamizi la kutogombea nafasi hiyo
kwa awamu ya tatu, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi,
amesema kinachotokea kwenye chama hicho ni matokeo ya kupuuza ushauri
wake.
Mbowe amewekewa pingamizi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa
Tabora, Kansa Mbarouk, ambaye pia ni mgombea wa nafasi hiyo, kwa madai
ya kukiuka katiba ya chama hicho na maagizo ya msajili wa vyama vya
siasa.
Akizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam jana, Jaji Mutungi alisema
kuwa ofisi yake iliwashauri viongozi wa chama hicho kuhitisha mkutano
wa Kamati Kuu ili waweze kufanya marekebisho ya Katiba yao kabla ya
uchaguzi, lakini walipuuza ushauri wake.
Alisema kuwa baada ya ushauri wake huo kupuuzwa, Mbarouk ameona fursa hiyo na kuamua kuitumia.
“Tuliwashauri Chadema muda mrefu kuhitisha mkutano wa Kamati Kuu ili
wafanye marekebisho ya Katiba yao, lakini walitupuuza na kuanza
kutulaumu. Kinachotokea sasa ni matokeo ya kile ambacho tulijua kinaweza
kutokea katika uchaguzi wao,” alisema Jaji Mutungi.
Alisema baada ya kuwaambia hayo, viongozi wa chama hicho waliishutumu ofisi ya msajili na kudai kuwa inatumika.
Jaji Mutungi alisema kutokana na hali hiyo, ofisi yake imeamua kukaa
kimya na kuacha mchakato wa uchaguzi uendelee, lakini mwishowe
wanatakiwa kuwasilisha taarifa zao katika ofisi hiyo.
“Tumeamua kuwaacha waendelee na mchakato wao, watavutana mwisho watachoka wakimaliza watatufuata,” alisema.
Mbarouk aliwasilisha taarifa yenye kumbukumbu namba Mbarouk/UCH/14
kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chadema na Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo
inasema kuwa kufikia Septemba 14, siku ya uchaguzi mkuu wa chama hicho,
Mbowe atakuwa ametumikia vipindi viwili katika nafasi ya mwenyekiti
taifa.
Kulingana na Katiba ya Chadema kama ilivyothibitishwa na Msajili wa
Vyama vya Siasa, hakuna mwanachama anayeruhusiwa kuchaguliwa kuongoza
zaidi ya vipindi viwili katika cheo kimoja na ngazi moja.
Juni mwaka huu, msajili alidai kuwa Mbowe hawezi kuwania nafasi hiyo
kutokana na Katiba yao kuwa na kipengele cha ukomo wa uongozi wa vipindi
viwili.
Alisema ili aweze kuendelea na nafasi hiyo, alipaswa kuitisha mkutano wa
Kamati Kuu ili waweze kufanya marekebisho katika Katiba yao ikiwa ni
pamoja na kuondoa kipengele cha ukomo wa uongozi.
Katika hatua nyingine, chama hicho kimesema hakijapata taarifa za Mbowe kuwekewa pingamizi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho jana,
Mkurugenzi wa Kampeni na Uchaguzi, Singo Benson, alisema kulingana na
Katiba ya chama hicho walioomba kuteuliwa kama wana pingamizi au
malalamiko wanapaswa kupeleka ofisini, lakini hawajapokea hadi sasa.
“Sisi tumesoma tu kwenye magazeti, hatuna taarifa yoyote ya pingamizi
hadi sasa. Huyo anayesema alileta je, alilileta kwa njia gani na kama
‘dispatch’ ipo, aseme nani alipokea na kusaini,” alisema Benson.
Alisema ofisi ya chama hicho iko wazi muda wote na kwamba kwa siku ya
juzi alikuwapo ofisini hadi saa 5 usiku, lakini hakupokea pingamizi la
aina yoyote.
Wakati huo huo, chama hicho jana kiliwatangaza washindi wa uchaguzi wa Baraza la Wazee Taifa.
Nafasi ya mwenyekiti ilichukuliwa na Hashim Juma Issa kutoka Zanzibar,
Makamu Mwenyekiti Bara ni Suzan Lyimo na Makamu Mwenyekiti Zanzibar ni
Omar Masoud Omar.
Wengine ni Rodrick Lutembeka ambaye alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu na Erasto Gwota aliyechaguliwa kuwa Mweka Hazina
No comments:
Post a Comment