MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete amefanyiwa upasuaji wa tezi dume (Prostate) katika hospitali ya Johns Hopkins iliyopo katika jimbo la Maryland nchini Marekani.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa mawasiliano Ikulu Salva Rweyemamu katika vyombo vya habari jana imesema Rais amefanyiwa upasuaji huo juzi alfajiri baada ya madaktari waliomfanyia uchunguzi wa afya yake kujiridhisha kuwa alikua anahitaji matibabu ya aina hiyo.
“Upasuaji huo ulifanyika alfajiri na kuchukua muda wa saa moja na nusu,umefanyika salama na kwa mafanikio makubwa na bado yupo wodini akiendelea vizuri chini ya uangalizi wa madaktari na kupatiwa tiba,”alisema Rweyemamu.
Wiki iliyopita Kurugenzi hiyo ya mawasiliano ikulu ilitoa taarifa ya Rais kwenda Marekani kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake na kuwa angekaa huko kwa siku 10.
MWANANCHI
Walimu wawili wa Shule ya Sekondari ya Embarway wanashikiliwa na Polisi Wilayani Ngorongoro wakituhumiwa kufanya mitihani ya kidato cha nne ofisini.
Licha ya walimu hao kukamatwa pia walikua wasimamizi wa ndani wa mitihani kwenye shule hiyo wameondolewa kutokana na uzembe.
Kaimu Ofisa elimu wa Wilaya ya Ngorongoro Chama Magewa alidai walimu hao Jacob Jaddie na Reginald Boniface walikamatwa wakiwa wanafanya mtihani wa historia na walikamatwa na msimamizi mkuu wa mitihani hiyo baada ya kuingia gafla kwenye ofisi ya mwalimu mkuu.
“Msimamizi alikua anafuata moja ya fomu kwa ofisi ya mwalimu mkuu,baadaye aliita Polisi na kuwakamata watuhumiwa hao”alisema.
MWANANCHI
Waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa amesema hana mpango wa kutangaza nia ya kugombea urais kwa sasa,bali anapenda kushirikiana na waumini na wananchi katika shughuli za maendeleo.
Alisema hayo katika uzinduzi wa helikopta ya kanisa la ufufuo na uzima,Dar es salaam jana.
“Nilipofika hapa kuna mmoja wa rafiki zangu akaniuliza umekuja kutangaza nia?nikamwambia sikuja kutangaza nia hapa…sina mpango huo kwa sasa,nimekuja kusali na kushiriki kanisani kwa ajili ya kuinua jina la Bwana,”alisema Lowassa.
Alisema Taifa linahitaji viongozi wenye maono ambao ndio wanaoweza kulivusha na kulipeka mbele kwa kuwa wataleta mabadiliko chanya.
NIPASHE
Chama cha demokrasia kimemshtaki aliyekua Mwenyekiti wa Bunge maalum la Katiba Samuel Sitta kwa wapiga kura wake wa Urambo Mashariki kuwa alishiriki kuchakachua maoni ya Watanzania katika mchakato wa kuandika katiba mpya.
Chama hicho kimesema kuwa walimuamini sana Sitta na kumchagua Mwenyekiti wa Bunge hilo ambaye angesimamia kupatikana kwa katiba bora na yeye kuzingatia maslahi ya Taifa,lakini aliwasaliti na kuchakachua maoni ya wananchi wengi.
Mbowe alisema mchakato wa kuipata Katiba mpya ulitokana na kelele zilizopigwa na Chadema ikiwemo kutishia kuandama kuidai,hali iliyomfanya rais kusikia kilio chao na kuamua mchakato huo ufanyike kwa mustakabali wa Taifa.
Mbowe aliwataka wananchi wa Urambo kutomchagua Sitta kuwa Mbunge wao katika uchaguzi mkuu ujao kwa madai kuwa ameshindwa kuwaletea maendeleo,aidha aliwataka kuacha kuikumbatia CCM kwa kuwa imeshindwa kuwaletea maendeleo huku wakulima wa mpunga na Tumbaku wakilalamika na badala yake wachague wapinzani ili wawaletee maendeleo.
NIPASHE
Harakati za kuwania urais ndani ya Chama cha Mapinduzi CCM katika uchaguzi mkuu ujao zimeanza kumletea shida Waziri mkuu Mizengo Pinda baada ya wajumbe wa UVCCM kudai kupinga vikali pendekezo la kutaka ateuliwe kuwa Naibu kamanda wa Umoja huo Tanzania bara kwa madai kwamba hana sifa.
Pinda anadaiwa kukumbana na pigo hilo katika vikao vya Baraza hilo vilivyofanyika November 7 hadi jana mjini Dodoma vikiwa chini ya Mwenyekiti Sadifa Juma.
Baadhi ya wajumbe hao walisema wajumbe walipinga pendekezo la uteuzi wa Pinda kwa madai kuwa hana sifa huku baadhi ya vigogo wa UVCCM wakituhumiwa kuhusika na rushwa ili kusuka mpango huo.
Baada ya kuvuja kwa taarifa juu ya pendekezo la kutaka pinda ateuliwe kushika nafasi hiyo,wajumbe wengi walijiandaa kikamilifu kulipinga kwenye kikao cha Baraza kuu.
HABARILEO
Ulaji wa supu ya pweza,karanga mbichi,mihogo mibichi na mbata kwa madai kwamba vinaongeza urijali kwa wanaume kumeelezwa kuwa ni dhana potofu inayostahili kupigwa vita kwa kuwa haina uhusiano kati ya urijali wa mwanaume na vyakula hivyo.
Kauli hiyo imetolewa na Dk.Cuthbert Maendaenda wakati akitoa mada yake kwenye semina ya wahariri iliyofanyika Morogoro iliyojadili nafasi ya mwanaume katika kuleta mabadailiko katika jamii juu ya afya ya uzazi na jinsia.
Alisema katika miji mingi kwa sasa supu ya pweza huuzwa ambapo wauzaji wamekua wakinadi kama msaada wa kurejesha heshima ndani ya jamii.
Alisema ufanyaji mapenzi unaathirika na vitu vingi na jamii lazima kuangalia ukweli huo ili kuwa na watu wanaojiamini katika mapenzi na wale ambao wana matatizo kupata ushauri wa kidaktari.
HABARILEO
Takribani wanawake 1500 hufariki dunia kila mwaka kutokana na utoaji mimba usio salama nchini huku asilimia kubwa ikiwa ni vijana.
Mkurugenzi wa Marie Stopes Tanzania Ulla Muller alisema mbali na idadi kubwa ya watu kupoteza maisha,wanafunzi wa kike 8,000 wanalazimika kuacha shule kila mwaka kutokana na kupata ujauzito huku wanafunzi 1,750 wakifukuzwa shule za msingi kwa tatizo hilo.
Muller alisema ili kukabiliana na tatizo hilo ipo haja ya kutambua na kuboresha upatikanaji wa huduma ya uzazi wa mpango kwa vijana huku akimpongeza Rais Kikwete kwa kutambua mchango wa kutoa kipaumbele katika suala hilo na kuahidi kuongeza matumizi ya uzazi wa mpango.
MTANZANIA
Mwanafunzi Jenipher Leornad mwenye miaka17 aliyemaliza darasa la saba katika shule ya msingi Shanwe iliyopo Mkoani Katavi amejiua kwa kunywa aina mbalimbali za dawa na mafuta ya taa baada ya kufeli mtihani wa darasa la saba huku mdogo wake akifaulu.
Kaka wa marehemu Masumbuko Leornard alisema Jenipher alifariki juzi usiku muda mfupi baada ya kufikishwa hospitali ya Wilaya ya Mpanda.
Alisema marehemu alikua akisoma na mdogo wake walikua wamekaa nyumbani na mmoja wa wanafunzi waliyehitimu nae darasa la saba aliwaletea taarifa za matokeo yao na kwamba matokeo hayo yanaonyesha Jenipher amefeli na mdogo wake amefaulu.
“Baada ya kuambiwa hivyo Jenipher hakuamimni na kuamnua kwenda kuangalia mwenyewe kwenye mtandao wa baraza la Mtihani na alipofika huko alikuta matokeo kama aliyoambiwa na mwenzake na alirudi nyumbani na kumweleza mdogo wake aliyefaulu kuwa anaona aibu kwa sababu yeye ni mkubwa na amefeli,’Alisema kaka wa marehemu.
Alimwambia mdogo wake ni bora anywe sumu kuepuka hiyo aibu na ndipo alipoingia chumbani kwa mama yake na kuamua kukusanya vidonge vya aina mbalimbali vya dawa za binadamu kisha kunywa na mafuta ya taa ambapo alifariki muda mfupi kabla ya kufikishwa hospitali.
MTANZANIA
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Shy-Rose Bhanji amesema kuwa atawachukulia hatua za kisheria wabunge wenzake wanaomzushia tuhuma za kutoa lugha chafu,ulevi wa kupindukia na kuwatukana baadhi ya marais wa Jumuiya hiyo.
Akizungumza jana Shy-Rose alisema baadhi ya Wabunge hao wamemzushia kwamba alifanya vurugu na kuvunja chupa ndani ya ndege na hatimaye kufungwa pingu wakati wa ziara ya wabunge hao nchini Ubelgiji.
“Madai haya yote hayana ukweli wowote na yanalenga kuniharibia sifa yangu ya utendeji kazi katika bunge la Afrika Mashariki na lengo lao ni kunivunjia ari ya kutetea maslahi ya Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla,”Alisema Bhanji.
Alisema pamoja na kutuhumiwa huko lakini wahusika wameshindwa kufuata taratibu ambazo ni kupelekwa kwenye kamati ya uongozi ya Bunge yenye mamlaka ya kushughulikia jambo hilo.
MTANZANIA
WANANCHI wa kata ya Nyakafuru Mkoani Geita wameiomba Serikali kufunga Zahanati ya kata hiyo iliyojengwa kwa gharama ya shilingi milioni82.
Wananchi hao walilalamikia kitendo cha zahanati hiyo kutofunguliwa licha ya kukamilika kwa mwaka mmoja uliopita.
Aidha wananchi hao walilaumu viongozi wao kwa kushindwa kuwapa taarifa ya kutofunguliwa kwa zahanati hiyo kwani wanapata shida kutembea mwendo mrefu kufuata huduma sehemu nyingine.
MTANZANIA
Mtoto mmoja Wilayani Serengeti Mkoani Mara anatuhumiwa kumuua mwenzake wa miaka 13 ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Kibeyo.
Inadaiwa mauaji hayo yalifanyika kwa kutumia sime wakati watoto hao walipokua wakichunga ngo’mbe,
Mganga mkuu Hospitali ya Nyerere alithibtisha kifo cha mtoto huyo na kueleza kuwa walipokea mwili wa marehemu November7 saa11 jioni.
Dk Mwasha alisema baada ya kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu madaktari walibaini kwamba alikua amekatwa na kitu chenye ncha kali na kuathiri ubongo wake na hivyo kusababisha damu nyingi kuvuja katika ubongo
No comments:
Post a Comment