Monday, 13 January 2014

CHAMA KIPYA CHAJA, WALIOFUKUZWA UPINZANI WATAJWA.

 
WAKATI fukuto la kufukuzwa uanachama kwenye Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) likiwa bado bichi, chama kipya cha siasa kimeanzishwa na watu wanaodaiwa kuwa ni muungano wa wanachama waliofukuzwa kutoka vyama vya upinzani nchini.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa nchini, zinakitaja chama hicho kuwa ni African Alliance for Change and Transparence (AACT) na kwamba mipango ya usajili wa muda wa chama hicho inadaiwa kuanza kuratibiwa kwa takribani mwezi mmoja sasa.

MTANZANIA Jumapili limedokezwa kuwa, tayari chama hicho kimekamilisha baadhi ya taratibu na kinatarajiwa kupewa usajili wa muda na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa siku ya Jumanne, wiki ijayo.

Gazeti hili limedokezwa kuwa iwapo chama hicho kitapata usajili huo, upo uwezekano wa wanachama waliofukuzwa uanachama kutoka Chadema hivi karibuni kujiunga na chama hicho.

Wanasiasa wengine wanaotajwa ama kuwa nyuma ya kuanzishwa kwa chama hicho au wanatarajia kujiunga, ni wale waliofukuzwa kutoka CUF, nia ikiwa ni kuendeleza harakati zao za kisiasa.

No comments: