Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue akitangaza mabadiliko ya Baraza la
Mawaziri katika mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana,
Picha na Edwin Mjwahuzi
Dar es Salaam. Rais
Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri ambayo
yamewatupa nje mawaziri watano, kuwaingiza 10 wapya, kuwapandisha
manaibu wanne kuwa mawaziri kamili na kuwahamisha wengine wanane kutoka
wizara zao kwenda nyingine.
Miongoni
mwa walioachwa katika mabadiliko yaliyotangazwa jana na Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue jana, ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu
wa Rais (Mazingira), Dk Terezya Huvisa ambaye nafasi yake imechukuliwa
na aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji, Dk Binilith Mahenge.
Wengine
walioachwa na wizara zao kwenye mabano ni Manaibu Waziri, Goodlucky Ole
Medeye (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Gregory Teu (Viwanda na
Biashara), Benedict Ole Nangoro (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) na
Philipo Mulugo (Elimu na Mafunzo ya Ufundi).
Mawaziri
hao wanaungana na waliokuwa mawaziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel
Nchimbi, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha,
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David na Maliasili na Utalii,
Khamis Kagasheki ambao uteuzi wao ulitenguliwa na Rais kutokana na
matokeo ya uchunguzi wa Kamati ya Bunge kuhusu utekelezaji wa Operesheni
Tokomeza Ujangili.
Balozi
Sefue alisema kuachwa kwa mawaziri hao ni moja ya hatua zilizochukuliwa
na Rais Kikwete kuimarisha utendaji serikalini. Pia alisema mabadiliko
hayo yametokana na kuwapo kwa nafasi baada ya kutenguliwa kwa uteuzi wa
mawaziri hao na kifo cha aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa.
“Rais
amefanya mabadiliko kwa mujibu wa Ibara ya 55 (4) ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania inayompa mamlaka ya kutekeleza wajibu huo,”
alisema Balozi Sefue.
Sura mpya
Sura
10 mpya zilizoingia katika Baraza hilo ni pamoja na Dk Asha Rose Migiro
aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mbunge wa Busega, Dk
Titus Kamani ambaye anakuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na
Naibu wake, Kaika Saning’o ole Telele ambaye ni Mbunge wa Ngorongoro.
Wengine
wapya ni wale walioteuliwa kuwa Naibu Mawaziri na wizara zao kwenye
mabano, Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba (Fedha), Mbunge wa
Viti Maalumu, Pindi Chana (Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto) na
Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama (naibu wairi Elimu na Mafunzo ya Ufundi) kushoto na Mbunge wa songea mjini Emanuel Nchimbi aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani
Pia
wapo Mbunge wa Serengeti, Dk Steven Kwebwe (Afya na Ustawi wa Jamii),
Mbunge wa Mbozi Magharibi, Godfrey Zambi (Kilimo, Chakula na Ushirika),
Mbunge wa Mufindi Kusini, Mahmoud Ngimwa (Maliasili na Utalii) na Mbunge
wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo).
Waliopandishwa, kuhamishwa
Mbali
na Dk Mahenge, Rais Kikwete pia amewapandisha manaibu waziri wengine
watatu kuwa mawaziri kamili pasipo kuwahamisha wizara walizokuwa. Hao ni
Saada Nkuya Salum anayekuwa Waziri wa Fedha, Lazaro Nyalandu (Maliasili
na Utalii) na Dk Seif Rashid (Afya na Ustawi wa Jamii).
Balozi
Sefue alisema Rais Kikwete amewahamisha aliyekuwa Waziri wa Katiba na
Sheria, Mathias Chikawe kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuchukua
nafasi ya Dk Nchimbi, wakati aliyekuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa
Jamii, Dk Hussein Mwinyi amerejeshwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa, kuchukua nafasi ya Nahodha. Dk Mwinyi aliwahi kuongoza
wizara hiyo.
Wengine
waliohamishwa ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia
na Watoto, Ummy Mwalimu kwenda kuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Makamu wa Rais, kuchukua nafasi ya Charles Kitwanga aliyehamishiwa
Wizara ya Nishati na Madini kuendelea na wadhifa huo. Kitwanga anachukua
nafasi ya George Simbachawene ambaye amehamishiwa Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
No comments:
Post a Comment