Friday 10 October 2014

MADEREVA WA MABASI YA UDA WAGOMA, ABIRIA WALAZIMIKA KUTEMBEA KWA MIGUU.

Na Mwandishi wetu
MADEREVA wa Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (UDA), wanaofanya safari kati ya Mnazimmoja na Kivukoni jana waligoma kufanya kazi wakipinga agizo la uongozi kuwataka wapeleke hesabu ya sh 300,000 kwa siku.
Kutokana na mgomo huo abiria wanaosafiri katika njia hiyo, walipata usumbufu hadi pale ufumbuzi wa mgogoro huo ulipopatikana majira ya saa moja asubuhi.
Akizungumza niaba ya madereva na makondakta jijini Dar es Salaam, mmoja wa madereva, ambaye hakupenda jina lake liandikwe kwenye mtandao huu wa eddy blog, alisema, wamekuwa wakifanya kazi katika manyanyaso makubwa kuhusu hesabu.
Alisema sababu zilizowafanya wagome zimetokana na ukweli kwamba kutokana na ushindani wamagari katika njia hiyo, wanauhakika fedha hizo haziwezi kupatikana kirahisi.
“Sisi tunaulaumu uongozi wa kampuni hii kwani umekuwa ukiendeshwa kikabila na mabavu, pindi wafanyakazi tunapo hoji haki zetu za msingi,”alisema dereva hyo.
Alisema baada ya uongozi kupata taarifa kuwa wamegoma, alifikia mmoja wa viongozi katika eneo la Mmnazimmoja ambako walikuwepo madreva hao na kuwashawishi waanze kazi kwa kutumia hesabu ya awali ambayo ni sh 205,000.
Hata hivyo kiongozi huyo, aliwashangaza madereva hao pale alipowaambia kuwa wataanza kukusanya hesabu hiyo y ash 300,000 baada ya kuzisimamisha kampuni nyingine zinazotoa huduma hiyo katika njia hiyo.
“Unajua watu wakituona hivi wanajua tunalipwa vizuri kumbe wala sio hivyo kwa mfano makondakta wote hawakuajiriwa, tulioajiriwa ni sisi madereva ambao hata mshahara wenyewe hatuupati kwa wakati huku tukitakiwa kununua sare za kazi na kupeleka sh 5000 ya kuoshea gari kila siku,”alisema.
Aliongeza kuwa viongozi wa kampuni hiyo wamekuwa mara kwa wakitoa lugha za vitisho za kumfukuza kazi kila mfanyakazi anayepingana na maamuzi ya uongozi hata kama unakandamiza haki zao.
Akizungumzia kuhusu ajira katika kampuni hiyo, alisema kwa kuwa kiongozi mkuu wa kampuni hiyo anatoka Kanda ya Ziwa, hivyo nafasi nyingi za ajira zimekuwa zikienda kwa kabila la wasukuma.
Alipotafutwa msemaji wa UDA, George Maziku, kuyatolea ufafanuzi malalamiko hayo, alisema madereva wote waliojaribu kugoma wamewaondoa na kuwapeleka njia nyingine kauli ambayo imetofautiana na madereva.
Akisema madereva waliopelekwa baada ya kuondolewa hao waliopinga wamekubali kupeleka hesabu y ash 300,000.
“Kuhusu suala la ukabila huyo dereva aliyesema hivyo ni mpumbavu kama yeye siyo msukuma ungemuuliza ameingiaje, na hili la kuondolewa kampuni nyingine katika njia hii, hili halina ukweli wowote,”alisema Maziku.

No comments: