Tuesday 8 July 2014

YA MAKAMBA NA URAIS

 http://www.mwananchi.co.tz/image/view/-/1689972/highRes/460607/-/maxw/600/-/156ucvh/-/makamba.jpg
 
 
Kauli ya Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, kwamba, Tanzania inahitaji kiongozi kijana katika nafasi ya urais mwenye fikra mpya katika uchaguzi mkuu ujao, imeelezwa kuchochea mtafaruku ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa.

Katibu Mwenezi wa Itikadi na Siasa wa (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Charles Shigino, alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jana.Alisema usemi huo ni kuleta siasa za ubaguzi ndani ya chama. 
Shigino alisema CCM inapiga vita ubaguzi wa aina yoyote ndani ya chama na kuongeza kuwa kauli ya Makamba ni silaha tosha ya kukivuruga chama, hivyo anapaswa kuomba radhi.
 


“Kauli ya Makamba siyo ya kiungwana. Nadhani aliropoka, hakufikiria anachokisema. Na katika nchi hii ndiyo imekuwa ikiongozwa na wazee ndani ya miaka mingi na kuwa katika mstari mnyoofu.

Hivyo, wazee wanapaswa kupewa heshima zao na kijana huwezi kufanya jambo la maana bila ya kuwa na mzee nyuma yako,” alisema.
Aliongeza: “Katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia siyo kwamba, nchi ndiyo itawaliwe na vijana tena katika nafasi nyeti ya urais. Makamba anatakiwa kujitathmini mara mbili mbili. Wazee ndiyo nguzo ya nchii hii. Wanaifahamu tokea enzi za uhuru. Sisi tumekuta historia tu.”


“Kama kweli Makamba kama ana nia ya urais, ni bora akajipa muda wa kujifunza na kupata uzoefu wa kutosha wa nafasi ya uongozi katika nafasi hiyo. Kwani Watanzania wanajua bila ubishi kuwa katika nafasi ya uongozi ndani ya CCM hana muda wa mwaka mmoja na nusu.”

Alisema kisiasa Makamba bado ni mdogo na kwamba, anatakiwa kwenda kujifunza kutoka kwa wazee waliopo ndani ya CCM, ambao yeye amekuwa akiwadharau.
Shigino alisema Makamba anatakiwa kujua kuwa Watanzania wanapomchangua mgombea urais kupitia CCM ndiye huyo huyo atakayekuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa.
Alisema kwa sasa taifa lilipofikia linatakiwa kuongozwa na kiongozi mwenye maamuzi ya kutosha pamoja na uzoefu wa kukabiliana na changamoto zilizopo, hasa katika nyanja ya uchumi, mendeleo ya jamii pamoja na siasa yenye utawala bora.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: