Serikali
ya Tanzania iko hatarini kukosa dola za Marekani milioni mia saba sawa
na trilioni 1.1 kwa fedha za Tanzania kwa ajili ya mradi wa pili wa
mfuko wa changamoto za Milenia (MCC) kutokana na kushamiri kwa vitendo
vya rushwa nchini humo.
Marekani imebainisha kuwa mkataba wa pili
wa miradi inayofadhiliwa na shirika lake la Changamoto za Milenia (MCC)
utategemea hatua zitakazochukuliwa na serikali ya Tanzania dhidi ya
wahusika wa kashfa hiyo.
Haya yanajiri wakati Rais Jakaya Kikwete
akisubiriwa kutoa maamuzi ya mapendekezo yaliyofikiwa na Bunge kuhusiana
na sakata la uchotwaji fedha zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka kaunti ya
Tegeta Escrow wiki ijayo.
Katika tamko hilo kwa umma ambalo
limewekwa kwenye tovuti ya MCC, bodi ilieleza kutambua umuhimu wa
kusubiri na kuona utekelezaji kamilifu wa tamko lililotolewa na Ikulu ya
Tanzania Desemba 9, mwaka huu kwamba itachukua hatua za haraka na kutoa
maamuzi dhahiri na thabiti kuhusu maazimio ya Bunge juu la suala la
IPTL.
Taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania
ilieleza kuwa wakurugenzi wa MCC waliokutana katika mkutano wao
uliofanyika Desemba 10, mwaka huu wamesikitishwa na hali ya rushwa
nchini Tanzania.
Uamuzi huo wa Marekani ambayo
inafadhili miradi mingi ya mabilioni ya fedha ni mtihani wa pili kwa
Rais Kikwete baada ya ule wa maazimio ya Bunge yaliyotaka viongozi
wakiwamo mawaziri waliotajwa katika kashfa hiyo kuwajibishwa.
Wanaotakiwa
kuwajibishwa na Rais Kikwete ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa,
Sospeter Muhongo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Profesa Anna Tibaijuka.
Wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Novemba
mwaka huu, Serikali ya Marekani kwa kupitia MCC, ilikubali kutoa ruzuku
ya hadi Dola za Kimarekani milioni 9.78 kwa ajili ya maandalizi ya
miradi ya uwekezaji yenye matokeo makubwa katika sekta ya nishati
nchini.
Tanzania ilikuwa mojawapo ya nchi kumi zilizojadiliwa na
Bodi ya MCC iliyokutana kuangalia kama nchi hizo zimekidhi vigezo vya
kuendelea na mchakato wa kuandaa mikataba mipya.
Wakati wa mkutano
wa 16 na 17 wa Bunge, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila
(NCCR-Mageuzi), alidokeza kusudio la Marekani kukataa kutoa fedha kwa
ajili ya miradi ya MCC, lakini Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo alikanusha taarifa hizo.
Juhudi za BBC kumtafuta
Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Mark Childress,aweze kuzungumzia juu
ya ripoti hiyo ziligonga mwamba kutokana na sababu za kiprotokali.
No comments:
Post a Comment